Siku chache tu baada ya kutokea shtuma za ufisadi katika idara ya mahakama, wito umetolewa kwa hatua kuchukuliwa ili kusafisha idara hiyo.
Usemi huo ulitolewa na mchungaji Benson Muiruri.
Akizungumza Jumapili katika kanisa la PCEA Dr Arthur, mchungaji Muiruri alisema kuwa ni jambo la kusikitisha kwa idara ya mahakama kuonekana kushamiri shtuma za ufisadi.
"Inakera sana kwamba idara ya mahakama ambayo inafaa kutoa mwelekeo pia inakosa mwelekeo na kushtumiwa kwa ufisadi"Muiruri alisema.
Wakati huo huo, alitoa wito kwa majaji wanaoshtumiwa kujihusisha na ufisadi kuondoka ili uchunguzi kufanyika.
Matamshi yake yanajiri wakati ambapo idara ya mahakama inashtumiwa kutokana na madai ya majaji kujihusisha na ufisadi.