Kukithiri kwa ufisadi nchini kumetajwa kama mojawapo ya maswala yanayo changia kuzorota kwa uchumi pamoja na kudidimia kwa sekta za biashara na maendeleo nchini.

Share news tips with us here at Hivisasa

Katibu wa Muungano wa Wafanyikazi wa Cotu, Kaunti ya Mombasa, amesema kuwa wengi wa wamiliki wa kampuni humu nchi wanakwepa kulipa ushuru, jambo ambalo alisema kuwa limekuwa changamoto kwa Halmashauri ya utozaji ushuru nchini KRA.

Akizungumza mjini Mombasa siku ya Jumatano, Gideon Mutiso alisema kuwa hatua hiyo imechangia pakubwa kwa halmashauri hiyo kushindwa kuwasilisha fedha za kutosha katika hazina kuu ya serikali.

Aidha, alisema kuwa ni lazima swala hilo likabiliwe kikamilifu.

"Kuna haja ya swala la ufisadi kukabiliwa kikamilifu nchini ili kuhakikisha Halmashauri ya KRA inafanya shughuli zake vyema kutokana na watu na makampuni ya kibiashara kulipa ushuru,” alisema Mutiso.

Wakati huo huo, Mutiso alishinikiza serikali kuvifufua viwanda vya Pwani kama kile cha Sukari cha Ramisi, kiwanda cha Korosho Kilifi, ili kuhakikisha kuwa vijana wanapata nafasi za ajira.