Ufisadi, ukosefu wa mipangilio thabiti wa miradi ya kimaendeleo na mivutano ya kisiasa imetajwa kama baadhi ya mambo yanayolidurisha taifa nyuma kiuchumi.
Mwenyekiti wa kitaifa wa wadau katika sekta binafsi nchini KEPSA, Dennis Awori amesema ipo haja ya bunge la kitaifa kuweka mikakati dhabiti itakayozikabili changamoto zinazodunisha uchumi wa nchi.
Akizungumza mjini Mombasa siku ya Ijumaa, katika kongamano la kibiashara, Awori aliitaka serikali kuibuka na mbinu bora zaidi zitakazoleta ushindani wa kiuchumi kwa lengo la kuafikia ruwaza ya mwaka wa 2030.
“Tunamaono ya ruwaza ya mwaka wa 2030 yatakayoboresha uchumi wa taifa hili, lakini tutafanikiwa tu iwapo tutashirikiana na kudhibiti ufisadi na siasa potovu,” alisema Awori.
Kwa upande wake, Spika wa bunge la kitaifa Justin Muturi alisema kuwa bunge hilo tayari limepitisha sheria zinazotoa nafasi kwa sekta binafsi kuchangia katika kukuza taifa.