Bodi ya Elimu katika wilaya ya Nyamache, eneo bunge la Bobasi kaunti ya Kisii imesimamisha rasmi kufunguliwa kwa shule mpya za sekondari katika eneo hilo hasa shule za kibinafsi.

Share news tips with us here at Hivisasa

Akiongea katika kikao cha maafisa wa elimu kilichoandaliwa katika mji wa Nyamache, mwenyekiti wa bodi hiyo ya elimu eneo hilo, Stanley Too, alisema hili litasaidia kufanya uchunguzi zaidi na kwa kina kwa shule zote katika eneo hilo.

Hili pia ni kuhakikisha kuwa shule zinafuatilia masharti ya wizara ya elimu kikamilifu, la sivyo zitafungwa mara moja.

Haya yanajiri baada ya baadhi ya shule kukosa vitu muhimu kama maji, mabueni ya kutosha ambapo msongamano wa wanafunzi unashuhudiwa.

Kwingineko, wanafunzi wa  shule za msingi katika eneo bunge la Bomachoge Chache  walipata afueni kubwa baada ya mhisani mmoja kuwapa viatu.

Nyangena Omanga, akishirikiana na shirika la msalaba mwekundu, alisaidia shule kama Nyamiobo, Itare, Nyakoiba na Kebera huku shule zingine kama Nyabioto Riteka na Mesabakwa ambazo hazikufadhiliwa hiyo jana wakati wa kufunga mashule zikiahidiwa na mhisani huyo kufadhiliwa pindi watakapofungua shule juma la kwanza mwezi mei mwaka huu.