Viongozi wa kidini jijini Mombasa wameiomba serikali kuu kutoihusisha dini ya kiisalmu na matukio ya kigaidi.
Wakiongozwa na kiongozi wa msikiti wa Musa uliyopo maeneo ya majengo, Sheikh Abu Qatada, viongozi hao wamesema kuwa vitendo vya kigaidi vinatakelezwa na watu wanaoenda kinyume na mafunzo ya dini ya kiislamu, kwa hivyo serikali ipambane na mtu binafsi anayejihusisha na vitendo hivyo.
Aidha sheikh Qatada ameitaka serikali kuu kufanya kazi pamoja na viongozi wa kidini, mashirika ya haki za kibinadamu pamoja na wazee wa vijiji katika ukanda wa Pwani na sehemu zenginezo zinazokabiliwa na athari ya kujihusisha na imani kali.
‛‛Tayari tumeanza kuwasaidia vijana waliokuwa wameathiriwa na imani kali, tunatarajia polisi walinda usalama kutusaidia katika jambo hili, na wala sio kutumia nguvu zinazoweza kusambaratisha juhudi zetu katika kuwarekebisha vijana,’’ alisema.
Kiongozi huyo pia alishtumu vitendo vya serikali, kuwapoteza vijana wasiokuwa na hatia katika hali isiyoeleweka na wengine kuuliwa bila kwa kisingizio cha kuwa wanamgambo wa makundi ya kigaidi.
Akiongea katika msikiti huo wa Musa, Qatada ameitaka serikali kuja na njia muafaka ya kukabiliana na Ugaidi hapa nchini.
Sheikh Qatada sasa ndie mhuburi katika msikiti Musa uliokuwa umezungukwa na utata wa kujihusisha na visa vya kigaidi.