Msimamizi wa shirika lisilo la kiserikali la Health Care Rescue Centre Roseline Nyakona amesema ugonjwa wa saratani umekuwa nambari tatu kwa magonjwa mengine kwa kuwaua watu ulimwenguni.
Akizungumza siku ya Jumatatu katika Hospitali ya Rufaa ya Kisii iliyoko mjini Kisii, Msimamizi Nyakona alisihi watu kupimwa mapema na kila baada ya muda mfupi ili kujua hali zao kuhusu ugonjwa huo.
Aidha alisema kuwa kila mtu, awe mwanamke au mwanaume anastahili kupewa mafunzo jinsi ya kujipima ugonjwa huo na kuzuia maafa mengi dhidi yao wanapogundua kuwa wameathirika na kushughulikiwa mapema na madaktari kabla ugonjwa huo haujafika kwenye daraja la tatu.
“Naomba kila mtu awe akipimwa kila baada ya muda usio mrefu ili tuzuie maafa ya watu kutokana na ugonjwa huu na tutahakikisha kuwa tumeanzisha mafunzo kwa watu ili wajue jinsi ya kujipima,” alihoji Nyakona.
Wakati uo huo, watu walifurahishwa na matamshi ya msimamizi huyo huku wengi wakisema kuwa hiyo ni njia mojawapo ya kushughulikiwa kiafya kama wananchi.
“Wakiaanzisha mafunzo hayo tutaona kuwa sisi wananchi wa kawaida tumekumbukwa kwa matibabu na tutasema asante kwa msimamizi huyo,” alihoji Jane Onderi mmoja wa wakaazi wa Kisii.
“Tunasubiri mafunzo hayo tujue jinsi ya kujipima kabla ya ugonjwa huo kuenea ikiwa baadhi yetu tuko na ugonjwa huo,” aliongezea Cicilia Mose mkaazi mwingine.