Waziri wa afya katika kaunti ya Nyamira Gladys Momanyi amesema ugonjwa wa ukambi ni nambari tatu katika mauaji kote ulimwenguni.
Akizungumza mnamo siku ya Alhamisi mjini Nyamira, waziri huyo alisema ugonjwa huo ni miongoni mwa magonjwa mbaya yanayopotezea wengi maisha yao na kuna haja ya kuhakikisha watoto wamepata chanjo dhidi ya ugonjwa huo ili kutoathirika.
Wakati huo huo, Momanyi aliowaomba wazazi wote kuwapeleka wanao walio na umri wa chini ya miaka 14 katika hospitali za kaunti ya Nyamira ili kupata chanjo ya ugonjwa huo wa ukambi kwanzia tarehe 16 hadi tarehe 24 mwezi huu.
“Ugonjwa wa ukambi ni ugonjwa mbaya zaidi, naomba kila mzazi kuhakikisha mtoto wake amechanjwa dhidi ya ugonjwa huo ili kutoathirika,” alisema Momanyi.
Aidha, waziri Momanyi alisema serikali ya kaunti ya Nyamira inanuia kuwachanja watoto 276,000 dhidi ya ugonjwa huo.
Aidha, alisema hakuna kisa chochote cha ugonjwa wa ukambi kimerekodiwa katika kaunti ya Nyamira.