Wakazi wa Mombasa wanaotumia mafuta taa kupikia wanalazimika kutembea mwendo mrefu kutafuta bidhaa hiyo.
Bidhaa hiyo ambayo huitumia kwenye majiko ya kupikia wanasema imekosekana kwa kipindi cha wiki nzima kufikia sasa jambo ambalo limewalazimu kuzunguka mjini kutafuta bidhaa hiyo.
Kulingana na Charles Munya ambaye ni mhudumu wa kituo cha mafuta eneo la Kisimani eneo bunge la Nyali, bidhaa hiyo ilianza kuadimika mapema wiki hii huku wakazi wengi wakionekana kupanga foleni ndefu kuanzia asubuhi hadi jioni wakisubiri bidhaa hiyo.
Munya pia anasema kuwa mafuta taa katika kituo chake iliisha tangia siku ya Jumanne hali ambayo wengi wa wakazi wameonekana kughadhabika kwani kituo hicho ndicho kikubwa zaidi katika eneo la Kisimani ambacho kinaweza kutoa huduma hiyo kwa zaidi ya siku nne endapo vituo vyengine eneo hilo vimekauka.
Anasema kuwa sasa baadhi ya vituo vimepunguza vipimo kwa kuwa vituo vilivyosalia na mafuta ni kidogo ikilinganishwa na idadi ya wateja wanaokwenda kusaka bidhaa hiyo.
Juma Ramadhan ambaye ni mkazi wa Kisimani na anayetumia mafuta taa kupikia anasema kila atokapo kazini mwendo wa saa kumi na mbili jioni analazimika kuabiri gari hadi katika vituo vya mafuta huko mjini ndiposa aepukane na mlolongo mrefu wa wateja ambao anasema huongezeka kila dakika kwa kuwa wengi wa wakazi hutumia bidhaa hiyo kwa wingi.
Aidha mhudumu wa kituo hicho ameitaka wizara ya kawi kushuhulikia swala hilo kwani limewakosesha kazi kwa muda wa siku tatu kufikia sasa na anasema huenda ikafika jumapili kabla ya mafuta hayo kusafirishwa kwenye vituo mbalimbali.
Munya anasema tatizo sio fedha za kununua bidhaa hiyo kwenye hifadhi bali hua ni upungufu wa raslimali asili ya mafuta katika kituo kikuu cha changamwe.
Kwa upande wake mteja pia amesema kuwa serikali inapaswa kuingilia kati ili kupunguza misongamano ya watu wanaohitaji bidhaa hiyo sawia na kupoteza wakati wakitafuta mafuta hayo katika maneo ya mji.