Wakazi wa Kisimani eneo bunge la Nyali wamelalamikia ukosefu wa maji ambao umedumu kwa takribani mwezi mmoja kufikia sasa.

Is there a story unfolding in your community? Let Hivisasa know

Wakazi hao wamesema kuwa maji ya mifereji eneo hilo yamekuwa yakitoka mara moja kwa wiki huku mara nyengine yakikosekana kabisa jambo ambalo limewafanya kutumia maji ya chumvi kutoka kwa visima.

Kulingana na baadhi ya wakazi waliokuwa wameunga foleni katika kituo kimoja cha maji, mengi ya mabomba yakusafirishia maji eneo hilo yamepasuka huku yakichukua muda mrefu bila kukarabatiwa wala kubadilishwa.

Aidha wamesema kwamba mara nyingine mifereji hukauka jambo ambalo huwalazimu kununua maji kutoka kwa wachuuzi ambayo mara nyingi huwaletea maradhi ya kuharisha kwani wengi wa wachuuzi hawazingatii usafi wa mitungi wanayotumia kuhifadhia bidhaa hiyo.

Wakazi hao aidha wamesema kuwa mara nyingi huwalazimu kusubiri kwa muda mrefu ndiposa waweze kupata bidhaa hiyo jambo ambalo wamekiri kuwa linawapotezea wakati wakushuhulikia kazi maswala mengine katika familia.

Hata hivyo wameitaka bodi inayosimamia usambazaji wa maji kukarabati mabomba yote na kutafutia suluhu tatizo hilo kwani maji ni mojawapo ya bidhaa muhimu ambayo haipaswi kukosekana.