Shirika la kijamii la ‘Kenya Community Support Centre’ limesema kuwa kuchipuka kwa makundi ya kihalifu katika eneo la Kisauni, mjini Mombasa, kumechangiwa na hali ya vijana wadogo kujitosa katika utumizi wa dawa za kulevya.
Shirika hilo lilisema kuwa hali ya vijana wadogo kujitosa katika uhalifu ni kutokana na msukomo wa kupata dawa za kulevya kwa kuwa hawana pesa za kununua dawa hizo.
Akizungumza mjini Mombasa siku ya Jumatatu, afisa wa nyanjani wa shirika hilo Mwalimu Rama, alisema kuwa eneo la Kisauni linashuhudia msukosuko wa kiusalama huku wahusika wakuu wa hali hiyo wakiwa ni vijana wadogo ambao wamezama katika utumizi wa dawa za kulevya.
Mwanaharakati huyo wa kijamii katika Ukanda wa Pwani alisema kwamba iwapo tatizo hilo la utumizi wa mihadarati miongoni mwa vijana wadogo katika eneo hilo la Kisauni litadhibitiwa, basi swala la uhalifu litakuwa limekomeshwa.
"Lazima maswala ya vijana wadogo kujitosa katika utumizi wa mihadarati kukomeshwa ili kuwanasua vijana hao sambamba na kuimarisha usalama huo,” alisema Rama.
Kiongozi huyo wa kijamii, alisema kuwa ni lazima makundi hayo yakabiliwe na vijana hao wahusishwe katika miradi mbalimbali ya kimaendeleo katika eneo hilo, ili kuwakinga na uhalifu, kwani hali hiyo ina athari kubwa mno ya kiuchumi katika Kaunti nzima ya Mombasa.