Mji wa kitalii wa Ukunda umetajwa kuwa na rekodi ya juu ya utovu wa usalama.
Kamishna wa Kaunti ya Kwale Kutswa Olaka amesema kuwa mwaka huu pekee maeneo ya Ukunda na Diani yamerekodi visa vinane vya uhalifu.
Alifafanua kuwa miongoni mwa visa hivyo ilikuwemo mauaji ya wahudumu wa bodaboda yaliyotekelezwa na watu wasiojulikana.
Olaka alisema visa hivyo hutekelezwa katika vituo vya kujaza mafuta na maduka ya Mpesa, huku wanaotekeleza uhalifu huo wakisemekana kutumia pikipiki kutoroka.
Kamishna huyo alisema utovu wa usalama katika eneo la Pwani umeanza kuwa swala ambalo linastahili kuchukuliwa hatua za haraka.
Hapo awali, eneo la Kisauni katika Kaunti ya Mombasa, lilitajwa kama eneo linalokumbukwa na utovu wa usalama, kufuatia makundi ya uhalifu ya Wakali Kwanza na Wakali Wao kuhangaisha wakaazi wa eneo hilo.
Aidha, iliripotiwa kuwa wahudumu wa bodaboda wamekuwa wakilengwa sana na wahalifu hao, na hali inayopelekea wao kuwa na ugumu katika kutekeleza kazi yao.
Kamishna huyo alitoa onyo kwa magenge ya wahalifu wanaotekeleza vitendo hivyo kwa kusema kuwa chuma chao kimotoni kwa vile uchunguzi unaendelea.