Shughuli za kawaida zimekatizwa katika afisi ya wanachama wa Bandari ya Mombasa al maarufu Bandari Sacco, baada ya uhasama baina ya mkurugenzi mkuu wa chama hicho John Ogutu na mhasibu Moses Mugambi kutokea wazi wazi.

Do you have a lead on a newsworthy story? Share news tips with us here at Hivisasa!

Akizungumza na waandishi wa habari afisini mwake siku ya Alhamisi, Ogutu alidai kuwa bodi ya chama hicho imempa mapumziko ya lazima kwa kuwa amekuwa katika mstari wa mbele katika uchunguzi dhidi ya wanachama wa bodi hiyo, haswa Bwana Mugambi kuhusu sakata ya kupotea kwa takriban shilingi milioni nne ya chama hicho.

“Kuna fedha ambazo zimefujwa na maafisa wakuu wa chama hichi na mimi kama mkurugenzi mkuu nimekuwa katika mstari wa mbele kufanya uchunguzi wa ufujaji wa pesa haswa dhidi ya Moses Mugambi. Mhasibu huyo ameungana na wengine ili kunitimua kutoka afisini,” alisema Ogutu.

Hata hivyo, Mugambi alikanusha maadai ya kupotea kwa fedha zozote za chama hicho, kwa kusema kuwa mkurugenzi huyo hajatimuliwa kazini bali amepewa mapumziko ya lazima, ili uchunguzi ufanywe dhidi ya maadai kuwa yuko afisini kinyume na katiba ya chama hicho.

“Muhula wa mkurugenzi mkuu kuhudumu uliisha mwezi Juni mwaka jana, ila akajiongeza mwenyewe muhula wa miaka tatu kinyume na katiba. Ni vyema apumzike ili uchunguzi zaidi ufanywe kwa nini anakatalia afisini,” alisema Mugambi.