Wizara ya Mazingira na Mali asili inaunda mikakati ya kuhifadhi asilimia kumi ya misitu katika hatua ya kukabiliana na hali ya anga kwa kuhusisha jamii zinazoishi kandokando mwa misitu.
Kulingana na katibu katika wizara ya mazingira na mali asili Richard Lesiyampe, serikali inalenga kuhifadhi misitu yake nchini sawia na kuhakikisha kuwa haki za jamii wanaotegemea misitu kwa maisha yao ya kila siku imelindwa.
Akiongea mjini Nakuru, Lesiyampe amesema kuwa upungufu wa mikakati mwafaka kwa jamii zinapelekea uhaba wa vyakula sawia na kukauka kwa mito nchini
“Hapo awali, wizara ya mazingira ilikumbwa na changamoto ya kuweka sheria za kukabiliana na hali ya hewa kutokana na kukosa ufahamu kwa jamii ya Ogiek na Segwer, kuhusu haki zao kwa rasilimali za misitu kwani sasa kunaushirikianao kati ya jamii hizo na serikali,” alidokeza Lesiyampe.
Amehoji kuwa migogoro kati ya wananchi na Wanyama pori inaongezeka kila kuchao, kufuatia mbinu duni za kuhifadhi mazingira. Hata hivyo, amehoji kuwa kubadilika kwa minara ya misitu na maji itaimarisha maendeleo sawia na kupunguza visa vya migogoro miongoni mwa jamii
Hata hivyo, ameonya jamii zinazopigania kuishi kandokando mwa misitu dhidi ya uharibifu, akisema wanapaswa kukuza maendeleo na kujiingiza katika shughuli za kuongeza pato badala ya kusisitiza katika kuishi kandokando mwa misitu.