Aliyekuwa mwenyekiti wa chama cha TNA tawi la Nakuru  Abdul Noor, amemtaka rais Uhuru Kenyatta kufanya mazungumzo na vinara wa Cord ili kuzuia ghasia kuchipuka kutokana na misururu ya maandamano yanayoendelezwa na muungano huo kushinikiza makamishina wa tume ya IEBC kung’atuka afisini.

Share news tips with us here at Hivisasa

Akizungumza na mwandishi huyu mnamo Jumatatu, Noor alishangazwa na idadi kubwa ya maafisa wa usalama waliokuwa wakishika doria jijini Nairobi, wakati na kabla ya maandamano yaliyoongozwa na vinara wa Cord Raila odinga, Kalonzo Musyoka na Moses Wetangula.

“Ni kweli kwamba huenda IEBC ina udhaifu wake, lakini maandamano hayawezi kuleta suluhu. Ingekuwa bora kama wabunge wa Cord wangetumia nafasi yao bungeni kutoa changamoto kuondolewa kikatiba kwa IEBC. Suluhu la pili linaweza kupatikana ikiwa rais Uhuru atakubali kufanya mazungumzo na vinara wa Cord ili kuondolea taifa hali ya mshtuko."

Noor pia alisema ikiwa muungano huo hautasikizwa na kuendeleza maandamano hayo, huenda Kenya ikapoteza wawekezaji wa kigeni na hivyo kudidimia uchumi wa nchi.

Ameongeza kuwa taifa la Kenya huenda likaadhirika kiuchumi na kufufuka kwake huenda kutakuwa baada ya uchaguzi mkuu ujao mwakani 2018.

“Kwa sasa dunia nzima inatazama kile ambacho kinafanyika Kenya. Bila shaka tutawaogofya wawekezaji kuja hapa nchini kuanzisha biashara wakihofia usalama wao na mali yao,” alisema Noor.

Mwanasiasa huyo anayeegemea chama cha JAP, alisema kuwa vinara wa muungano huo wanafaa kupewa nafasi ya kupeleka malalamishi yao kwenye afisi za tume ya IEBC ili kuleta hali ya utulivu nchini.