Profesa Bogonko Nyachieo amesema kuwa Rais Uhuru Kenyatta atapata kura chache kutoka eneo la Gusii iwapo atazidi kushirikiana na Naibu wa Rais William Ruto.

Do you have a lead on a newsworthy story? Share news tips with us here at Hivisasa!

Nyachieo alisema kuwa wawili hao walizuru eneo hilo wiki iliyopita ili kuzindua miradi mbalimbali ya maendeleo lakini Bw Ruto akakosa 'kuomba msamaha' kuhusu machafuko ya baada ya uchaguzi wa mwaka 2007.

"Uhuru hatashinda uchaguzi katika eneo la Gusii iwapo ataendelea kushirikiana na Ruto. Huo ndio ukweli na matokeo ya mwaka 2017 yatathibitisha haya. Hawatafanikiwa hata wakizindua miradi mbalimbali katika eneo hili," alisema Nyachieo.

Aliongeza, "Ruto alikosa kuchukua fursa ya kujipatanisha na wakaazi na kuomba msamaha kwa sababu ya machafuko ya mwaka 2007/08, licha ya kesi yake kutupiliwa mbali na mahakama ya ICC.”

Alisema kuwa wenyeji wengi bado wanaamini kuwa Bw Ruto alichangia kwa wao kufurushwa kutoka eneo la bonde la ufa wakati wa vita hivyo.

"Sisemi kuwa yeye anahatia kwa sababu huo ni uamuzi wa mahakama. Ninachosema ni kuwa wananchi wanamlaumu kwa machafuko hayo. Hajachukua muda kufanya utafiti na cha kusikitisha ni kuwa wandani wake hawambii ukweli,” alisema Nyachieo.

Aliongeza, "Ruto na Rais Kenyatta walipaswa kuzungumzia suala la wakimbizi wa ndani ili kufanikisha maridhiano. Wakaazi wengi bado wanamlaumu Ruto kwa masaibu yao na fikra hizo hazitabadilika hivi karibuni iwapo hatasafisha jina lake. Bila kufanya hivyo, Kenyatta hawezi pata kura za eneo la Gusii.

Muungano wa Jubilee ulishindwa na Cord katika eneo la Gusii kwenye uchaguzi mkuu wa 2013, na unajibidiisha kubadilisha hayo.