Rais Uhuru Kenyatta na Rais wa Uganda Yoweri Museveni watakutana tena katika wiki mbili zijazo.
Mkutano huo utagusia maeneo yatakayowekwa mabomba ya kupitisha mafuta. Hii ni baada ya wao kutoafikiana kwenye mkutano waliokuwa nao siku ya Jumatatu.
Rais Kenyatta walikutana na mwenzake wa Rais Museveni siku ya Jumatatu kujadiliana kwa kina kuhusu ujenzi wa bomba lilopendekezwa la kupitisha mafuta kutaki nchi za Kenya na Uganda.
Hapo awali, msemaji wa ikulu ya rais, Manoah Esipisu alikuwa ametoa taarifa kwa usemi kuwa ujenzi wa bomba hilo utakuwa mwafaka bomba hilo likiwekwa maeneo ya kaskazini kupitia eneo la Lokichar hadi Lamu, jambo ambalo alisema litabadilisha miundombinu na maisha ya watu katika miji na kaunti za maeneo hayo.
Mkutano wa Jumatatu kati ya marais hao wawili pia ulihusisha maenyesho kutoka kwa washikadau husika katika sekta ya kawi ambao walieleza kuhusu mbinu bora ya kutumika kutekeleza mradi huo.
Hayo yalijiri huku mrengo wa ODM ukikashifu vikali ujio wa Museveni nchini Kenya huku wakisema kuwa ziara hiyo ya Museveni ni 'matusi' kwa nchi ya Kenya.
‘‘Tunamtaja Museveni kama kiongozi asiyekaribishwa nchini Kenya na tunamuomba akae mbali na tabia zake zisizofaa,’’ alisema Opiyo Wandanyi.
Wandanyi, ambaye pia ni katibu wa masuala ya siasa katika mrengo wa ODM, alisema kuwa Rais Kenyatta hafai kumkaribisha Museveni nchini iwapo wawili hao hawatajadili utata wa kisiwa cha Migingo.
Katibu huyo aliongeza kuwa kukaribishwa kwa Museveni nchini kumeashiria kuwa kisiwa cha Migingo kimeuzwa kwake na serikali ya Jubilee. Wundanyi alizidi kukashifu uongozi wa rais huku akisisitiza kuwa rais asiyeweza kutetea ardhi ya nchi yake hafai kusalia afisini.