Mwanasiasa mkongwe kutoka kaunti ya Nakuru Koigi wa Wamwere ameendeleza vita vyake vya kisiasa dhidi ya rais Kenyatta na naibu wake William Ruto.
Koigi alisema tangu wawili hao kuchukua usukani wa taifa, ufisadi umeongezeka maradufu.
“Watu walipomchagua Uhuru kama rais walifikiria kupigana na ufisadi itakuwa rahisi kwa sababu yeye ni tajiri, hata hivyo mambo yamegeuka na ufisadi hata umeongezeka,” Koigi aliandika kwenye ukurasa wake wa facebook.
Koigi, ambaye aliwahi kuhudumu kama mbunge wa Subukia, alisema Ruto na Uhuru wanafaa kuanzisha na kuendeleza vita dhidi ya ufisadi na wala si kuachia tume ya maadili na kukabiliana na ufisadi EACC pekee jukumu hilo.
“EACC haiwezi kuongoza vita dhidi ya ufisadi pekee,” Koigi alisema.
Aidha alishtumu serikali ya Jubilee kwa kile alidai ni uteuzi wa kikabila na hivyo kufanya baadhi ya makabila kutetea wafisadi kutoka jamii zao.