Mbunge wa zamani wa Subukia Koigi wa Wamwere, amesema Uislamu sio ugaidi, japo magaidi wanajificha katika dini ya Kiislamu, wakijifanya kutetea Waislamu, na imani yao pia.

Is there a story unfolding in your community? Let Hivisasa know

Koigi alisema hayo Jumatano akizungumza na Sauti Radio mjini Nakuru , baada ya Ubelgiji kushambuliwa Jumanne ambapo watu 31 waliuawa kwenye kituo cha treni na uwanja wa ndege Brussels kwa mabomu, ambapo amesema ugaidi sasa umedhihirika kama makabiliano ya itikadi ya kimagharibi dhidi ya jamii ya Mashariki.

“Ni lazima tutambue kwamba hivi sio vita vya wakristo dhidi ya waislamu, la hasha. Ni vita vya itikadi, na imani potovu, ambayo imekitwa ndani ya mawazo ya vijana maskaini kama wa matajiri, vijana wazungu kama wa kiafrika, kila mtu anaweza kuwa gaidi,” Koigi alisema.

Koigi alisema dhana ya ugaidi hutokana na hali kwamba baadhi ya watu duniani wanatafuta uhuru kutoka kwa wengine wanaowanyanyasa.

“Hata wakati Mau Mau walikuwa wanapigania Uhuru Kenya, waliitwa magaidi na wazungu ilhali walikuwa wakipigania uhuru wa Kenya na mali yetu. Wakati unaona kundi la watu limeingia katika ugaidi, mara nyingi wanapigania imani yao,” Koigi aliongeza.

Koigi alisema ugaidi ni kama “mtego wa panya unaoingia waliomo na wasio kuwemo” na kukabiliana nalo sio jukumu la taifa moja.

Watu wasiopungua 85 walijeruhiwa katika mashambulizi hayo ya Ubelgiji katika uwanja wa ndege wa Zaventem