Kamishna wa Kaunti ya Mombasa ametaja mpangilio duni wa majengo katika kaunti hiyo, kama sababu kuu inayotatiza juhudi za kukabiliana na visa vya uhalifu.
Kulingana na Maalim Mohammed, ujenzi wa kiholela umewafanya wenyeji wengi kutowafahamu vyema majirani wao, hali inayofanya washindwe kubainisha kati ya majirani wema na wahalifu.
“Ujenzi duni hapa Mombasa ndio unaochangia kujificha kwa wahalifu wengi, na kutupatia changamoto kukabiliana nao. Hatahivyo, tutazidisha juhudi zetu kuhakikisha kuwa usalama umeimarishwa,” alisema Maalim, wakati wa mkutano wa baraza mjini Mombasa.
Maalim sasa ameitaka serikali ya kaunti kuwajibikia suala la mpangilio wa ujenzi, ili kuiwezesha idara ya usalama kutekeleza wajibu wake vyema siku za usoni.
Afisa huyo wa utawala alilitaja eneo la Likoni kuwa kati ya maeneo yaliyoathirika zaidi na mpangilio duni wa majengo, unaotatiza juhudi za walinda usalama.