Mbunge wa Kisauni Rashid Bedzimba amelalamikia kile alichokitaja kama ujenzi mbaya wa nyumba katika kitongoji cha Mwandoni, hali aliyosema inachangia pakubwa kushuhudiwa kwa mafuriko katika eneo hilo.
Bedzimba alisema nyumba za eneo hilo zilijengwa bila kuzingatia utaalam na hali hiyo ndiyo inayosababisha mafuriko kila kunaponyesha.
Kauli ya mbunge huyo inakuja huku wakaazi wa kitongoji hicho wakikadiria hasara baada ya bidhaa zao kuharibiwa na maji ya mafuriko siku ya Jumapili.
Akizungumza na mwandishi huyu siku ya Jumapili alipozuru eneo hilo, Bedzimba alisema wanaendelea na juhudi za kutafuta suluhu la kudumu kuhusu tatizo hilo.
“Tunasikitika kwamba watu wameathirika lakini mimi kama kiongozi nimefika hapa kusaidia. Wale waliojenga hizi nyumba ndio waliofanya makosa kwa kuzijenga tu bila kutafuta sehemu ya kupitisha maji ya mvua,” alisema Bedzimba.
Aidha, mbunge huyo alidokeza kwamba wamiliki wa nyumba katika sehemu hiyo walipinga mpango wa kuchimba mitaro ya kupitisha maji na hali hiyo imetatiza pakubwa juhudi za kukabili janga hilo.
“Hapo awali tulikuwa na mpango wa kuchimba mitaro lakini wamiliki wa nyumba wakapinga mpango huo. Tutaleta wataalam wapime eneo hili ili tujue ni hatua gani tunapswa kuchukua,” alisema Bedzimba.
Baadhi ya wakaazi walipendekeza kutafuta makaazi mbadala ili kutoa nafasi kwa sehemu hiyo kufanyiwa ukarabati.