Mbunge wa eneo bunge la Nyaribari Masaba amesema ujenzi wa barabara ya Kiamokama-Keroka utaanza mwezi huu.

Is there a story unfolding in your community? Let Hivisasa know

Hii ni baada ya wakaazi wa eneo hilo kulalamika kuwa barabara hiyo ni mbaya.

Akiongea mjini Kisii katika harakati za kutembelea miradi ya eneo hilo siku ya Jumatatu, Bwana Elijah Moindi aliwataka wakaazi wa eneo Bunge lake kuwa na subira kwa vile mwanakandarasi aliyepewa kazi hiyo ameahidi kuanza kazi ya ukarabati wa barabara hiyo kabla ya mwisho wa mwezi huu wa Juni.

“Nitaendelea kushughulikia barabara zetu na lazima nitimize ahadi zote nilizotoa wakati wa kampeni za kuwania kiti hiki cha ubunge. Nawaomba wakaazi wa eneo langu la bunge wawe na subira kwani mambo mazuri ya maendeleo yanaanza,” alisema mbunge Moindi.

Mbunge huyo pia aliongeza kuwa atahakikisha kuwa vijana watapewa kipaumbele kufanya miradi yote katika bunge hilo, mojawapo ikiwa hiyo ya barabara hiyo ya Kiamokama kuelekea Keroka pamoja na ile ya Raitigo kuelekea Ekerongo hadi Nyamasibi.

Hizi ni mojawapo ya barabara ambazo mbunge huyo amesema zitakarabatiwa.

Naibu wa rais alipozuru eneo bunge hilo aliwaahidi wakaazi wa eneo bunge hilo kuwa kandarasi ya ukarabati wa barabara ilikuwa imetiwa kwenye ratiba ya ujenzi.