Gavana wa Kaunti ya Kisii James Ongwae amesema ujenzi wa chumba cha kuifadhi maiti katika Hostitali ya Rufaa ya Kisii ipo karibu kukamilika.
Akiongea mnamo siku ya Alhamisi katika mji wa Kisii, Ongwae aliwahakikishia wakaazi wa Kaunti hiyo kuwa ujenzi huo utakamilia hivi karibuni.
Haya yanajiri baada ya chumba cha kuhifadhi maiti cha zamani cha Hospitali hiyo kuyabeba maiti 40 pekee, jambo ambalo husababisha msongamano wa maiti katika chumba hicho na kuapelekea watu kulalama.
“Ujenzi wa Chumba cha kuifadhi maiti katika Hospitali ya rufaa ya Kisii utakamilika hivi karibuni na hakutakuwa na msongamano wa maiti kama ule unaoendelea kushuhudiwa katika chumba ambacho kinatumika kwa sasa katika Hospitali hiyo,” alisema Ongwae.
Wakati uo huo, Ongwae alikiri kuwa Serikali yake imeweka mikakati kabambe ya kuhakikisha zahanati zote katika Kaunti hiyo hazifungwi wakati wa wikendi na kufunguliwa kwa siku saba mfululizo ya wiki, hii ni baada ya baadhi ya zahanati kufungwa wakati wa wikendi jambo ambalo liliwapelekea wakaazi kutofurahishwa nalo, kwani ugonjwa haujui wikendi wala siku ya mapumziko.
“Zahanati zote zitakuwa zikifunguliwa siku zote ya wiki ili watu wawe wakihudumiwa kikamilifu kila siku, Serikali yangu itaangalia suala hilo na litafanyiwa marekebisho hivi karibuni,” aliongezea Ongwae.
Aidha, Ongwae alisema kuwa Serikali yake itawanunulia watu 800 kadi za matibabu za NHIF kwa kila Wadi ilioko katika Kaunti yake haswa wale ambao hawajiwezi kamwe huku akiwaomba wale wanaojiweza kujinunulia kadi hizo za matibabu ili huduma ya matibabu kurahisishwa kwa mahospitali.
Ikumbukwe kuwa Kaunti ya Kisii iko na Wadi 45 huku watu 36,000 wakifaidika na kadi hizo za matibabu za NHIF.