Gavana wa kaunti ya Kisii James Ongwae amewahakikishia wakaazi wa kaunti yake kuwa ujenzi wa chumba cha kuhifadhi maiti katika hospitali ya rufaa ya Kisii utakamilika hivi karibuni.
Kulingana na Ongwae alipoingia uongozini kama gavana wa kaunti hiyo mwaka 2013 alipata chumba hicho kikiwa kina uwezo wa kuhifadhi maiti 20 pekee jambo ambalo huwalazimisha wengi kuchukua wafu wao mapema na pia kusababisha msongamano katika chumba hicho.
Akiongea siku ya Alhamisi mjini Kisii Ongwae alisema chumba cha maiti ambacho kinaendelea kukarabatiwa kitabeba maiti 100 na kiko karibu kukamilika.
“Serikali yangu ilitenga pesa ili kujenga chumba cha maiti kipya maana kile kilichoko kwa sasa hubeba maiti ishirini na msongamono hushuhudiwa katika chumba hicho,” alikiri Ongwae.
Pia Ongwae aliwaomba wakaazi wa kaunti hiyo kushirikiana naye kuleta maendeleo mengi katika kaunti hiyo.
“Umoja hufanikisha maendeleo katika kaunti yetu naomba tushirikiane kuhakikisha maendeleo yako katika hospitali zetu, ukarabati wa barabara na mengine mengi,” aliongezea ongwae.