Wafanyabiashara wa Soko la Marikiti mjini Mombasa haswa wanaouza bidhaa za mapambo yenye asili za kipwani, wamesema kuwa ujenzi wa reli ya kisasa utainua viwango vya mapato kwao.

Is there a story unfolding in your community? Let Hivisasa know

Akizungumza siku ya Ijumaa katika soko hilo, Musa Massoud, anayetengeneza hereini na shanga alielezea imani yake kuwa reli hiyo itarahisisha namna ya kusafirisha mapambo hayo hadi katika kaunti nyengine ili kuyanadi kwenye masoko hayo.

Akilinganisha na usafiri wa magari, Ali alisema kuwa reli itawapa fursa ya kusafiri maeneo mbalimbali nchini ikizingatiwa kuwa ada yake ni nafuu, huku akiongeza kuwa tayari ukiwa ndani ya reli unaweza kuanza biashara yako kwani wageni wanaozuru taifa hili watakuwa wakitumia usafiri huo.

Kwa upande wake, Issa Karrimu anayefanya biashara ya kuuza mavazi ya Dini ya Kiisalamu almaarufu kanzu, pamoja na kofia, alisema kuwa ujenzi wa reli hiyo utazidisha mara dufu upanuzi wa biashara yake kwani itakuwa rahisi zaidi kuuza aina mbalimbali ya vazi hilo kwa waislamu wenzake hata katika nchi zingine.

Aidha, alisema kuwa biashara ya mavazi aina ya kanzu sio mavazi tu bali inalingana na vile yalivyoundwa ama yalivyoshonwa ndiposa yaweze kununuliwa kwa wingi.

Alisema biashara yake inatofautiana ikilinganishwa na wengine wanaouza vazi hilo huku akisema kuwa yeye mwenyewe hulishona kwa ustadi ili liweze kuwaridhisha wateja wake na hivyo basi kuweza kuwateka wateja zaidi kote nchini na hata katika mataifa ya Afrika Mashariki.

Hata hivyo, wafanyabiashara hao wameongeza kuwa iwapo reli ya kisasa ingekamilika kufikia mwaka huu, basi ingalikuwa bora zaidi kwa wao kupanua biashara zao ili ziweze kuafikia viwango vya kimataifa.

Ujenzi huo wa reli unatarajiwa kukamilika mwishoni mwa mwaka ujao.