Gavana wa kaunti ya Nyamira John Nyagarama amesema ujenzi wa soko la Mosobeti katika kaunti ya Nyamira ni bora, na kwamba ujenzi huo hautasimamishwa kamwe.

Share news tips with us here at Hivisasa

Hii inajiri baada ya baadhi ya viongozi na wakazi wa kaunti hiyo kuomba ujenzi huo kusimamishwa kwa kile walichokisema ni ujenzi usiozingatia mashariti ya ujenzi na msingi mbaya, jambo ambalo gavana amekanusha.

Akizunguimza siku ya Jumatatu katika soko hilo la Mosobeti alipotembelea ujenzi huo, Nyagarama alisema ujenzi huo unafanywa kulingana na masharti ya ujenzi.

“Wengi wamekuwa wakisema ujenzi wa soko hilo ni mbaya, lakini mimi mwenyewe nimetembelea ujenzi huo na nimeona kuwa ujenzi uko bora na hautasimamishwa kamwe,” alisema Nyagarama.

“Ni siku chache tu zimesalia ili ujenzi huo kukamilika maana kila kitu ni shwari, nimeona afisi ya soko na vyoo vya soko tayari vimekamilika na hivi karibuni soko yenyewe itakamilika,” aliongeza Nyagarama.

Tangu malalamishi kutolewa ujenzi huo kusimamishwa, ilikuwa siku ya kwanza kwa gavana Nyagarama kujitokeza na kutembelea ujenzi huo, huku akisema ni bora kuliko yale yanazungumziwa.