Ujenzi wa vibanda vipya unaendelea katika Soko la Kibuye jijini Kisumu, zaidi ya mwezi mmoja baada ya vibanda vya baadhi ya wafanyibiashara kuteketezwa na moto.
Moto huo ulisababisha hasara yenye thamani ya mamilioni ya pesa, huku jumla ya wafanyibiashara 289 wakiathiriwa.
Baada ya moto huo uliokisiwa kusababishwa na hitilafu ya nguvu za umeme, kamati ya wanachama tisa iliundwa ili kufanikisha ujenzi wa vibanda vipya kwenye soko hilo.
Kamati hiyo inajumuisha wafanyibiashara waliopoteza bidhaa zao kutokana na moto huo.
Mwenyekiti wa kamati hiyo, Christopher Otieno, alisema kuwa ujenzi huo unafadhiliwa na serikali ya Kaunti ya Kisumu, na unatarajiwa kukamilika katika kipindi cha juma moja lijalo.
“Ujenzi huu unafadhiliwa na serikali ya Kaunti ya Kisumu chini ya Gavana Jack Ranguma. Tunampongeza sana kwa ujenzi huu kwa sababu mikasa ya moto imekua ikitokea katika soko hili mara kwa mara lakini wafanyibiashara hawajawahi kujengewa vibanda,” alisema Otieno.
Stephen Ocholla, mwanachama wa kamati hiyo, aliitaka serikali ya Kaunti ya Kisumu kununua vifaa vya kuzima moto, ili kujiweka tayari kukabiliana na moto unapotokea kwenye soko hilo.
“Serikali ya kaunti ya Kisumu inafaa kuhakikisha kuwa soko hili ni la kisasa. Ujenzi wa vibanda vya mabati kwenye soko hili ndio chanzo cha mikasa ya moto ya mara kwa mara. Tunafaa kujengewa vibanda vya kisasa vilivyo na uwezo wa kustahimili moto,” aliongeza Ocholla.