Zoezi la kuwakagua maafisa wa polisi wanaohudumu katika kitengo cha trafiki kanda ya Pwani litaanza rasmi siku ya Jumanne mjini Mombasa.
Kwenye kikoa na waandishi wa habari mjini Mombasa siku ya Jumatatu, mwenyekiti wa Tume ya huduma kwa polisi nchini NPSC, Johnston Kavuludi, alisema kuwa zoezi hilo litachukua muda wa majuma mawili huku likilenga maafisa wa wanaoshikilia wadhifa wa constable.
“Kama tume tunalenga kuwakagua maafisa wa trafiki kwa kuwa wao ndio wanahakikisha kuwa hali katika barabara zetu inakuwa salama kwa wote wanazozitumia,” alisema Kavuludi.
Kavuludi vilevile alisema kuwa zoezi hilo linalenga kubaini utendakazi na uadilifu wa maafisa wa trafiki hasa kutokana na madai na tuhuma za mara kwa mara kuwa maafisa hao uhusika katika visa vya ulaji rushwa.
Aidha, Kavuludi aliwahimiza wananchi kushirikiana na tume hiyo kwa kutoa taarifa zozote muhimu kuhusiana na maafisa watakaohojiwa.
Kulingana na Kavuludi, takribani maafisa wa polisi 33 kati ya 1,566 waliokaguliwa kote nchini katika ukaguzi uliopita waliachishwa kazi baada ya kupatikana na kesi mbalimbali.
Takriban maafisa 238 wanatarajiwa kukaguliwa.