Ukahaba unaoendelezwa katika Kaunti ya Mombasa na maeneo mbalimbali ya ukanda wa Pwani umetajwa kuchangia ongezeko la familia za kurandaranda mitaani.

Share news tips with us here at Hivisasa

Akitoa kauli hiyo katika Kanisa la Holy Ghost Cathedral Mjini Mombasa, Askofu mkuu wa Kanisa Katoliki Jimbo la Mombasa Martin Kivuva, alisema kwamba tatizo hilo bado halijapewa mtazamo unaostahili.

Kivuva alisema kuwa hali hiyo imepelekea watoto wengi kuzaliwa na kutelekezwa na wazazi wao na hatimaye kuishia kurandaranda mitaani.

“Tatizo hili halijatiwa maanani kiasi cha kutafuta suluhu, ndio maana watoto hawa wameishia barabarani,” alisema Askofu Kivuva.

Vile vile, askofu huyo alisema ukosefu wa ajira pia umechangia ongezeko la familia hizo, ambazo alisema huishia kutumia dawa za kulevya na hata kujitosa katika magenge ya uhalifu.

Kivuva alisema sharti masuala hayo yazingatiwe, iwapo serikali za kaunti za Pwani zinalenga kulikabili tatizo la familia hizo zinazorandaranda mitaani.

Aidha, askofu huyo ameshauri wanandoa kuwa wavumilivu na kupokea nasaha kutoka kwa viongozi wa kidini wanapokumbana na misukosuko katika ndoa zao, ili kutotoa nafasi kwa ongezeko la familia hizo za mitaani.

Wakati huo huo, kiongozi huyo wa dini amesisitiza umuhimu wa wadau mbalimbali kujadiliana kuhusiana na swala hilo tata la familia zinazoishi mitaani.