Ukosefu wa mito ya kutosha na ukame unaoshuhudiwa umeathiri pakubwa kilimo cha ufugaji wa samaki katika eneo bunge la Bahati.
Baadhi ya makundi ya vijana yaliyojitosa katika kilimo hicho yamesema kuwa yanahofia kilimo chao huenda kikafifia, kutokana na ukosefu wa maji ya kutosha.
Wakiongea katika eneo la Kiamaina, vijana kutoka kikundi cha Kiamaina Youth Fish Farmers’ walisema kuwa ukame unaoshuhudiwa na ukosefu wa mto katika eneo hilo umewalazima kupunguza idadi ya vidimbwi vya samaki walivyokuwa navyo.
Walisema kuwa kisima walichokuwa wakitegemea kinaendelea kukauka kwa vile hakina kina kirefu.
“Tulikuwa na vidimbwi saba tulipoanza lakini tangu ukamae uanze mwezi Disemba mwaka jana tumelazimika kufunga vidimbwi vitatu kwa ajili ya ukosefu wa maji ya kutosha,” alisema Gregory Mwangi, Mwenyekiti wa kundi hilo.
“Hapa hatuna mto unaopita karibu na imekuwa vigumu kwetu kuwakimu hawa samaki bila maji ya kutosha,” aliongezea Mwangi.
“Tulikuwa na kisima lakini maji yameendelea kupunguka huko na sasa tunalazimika kununua maji kutoka kwa wachuuzi ili kujaza kisima hicho na hiyo ina gharama ya juu kwetu,” aliongeza kusema.
Irene Wairimu, mwekahazina wa kundi hilo la vijana alisema kuwa wanahofia watavifunga vidimbwi vyote iwapo ukame unaoshuhudiwa utaendeleakwa muda mrefu.
“Ni vigumu sana kumudu kilimo cha samaki bila maji na iwapo ukame utakithiri na tukose namana ya kupata maji basi huenda kukaachana na kilimo hiki na tuangazie shuguli zingine kwa sababu hata mazao ya samaki yamepungua kwa kiasi kikubwa sana,” alisema Wairimu.
Enoe bunge la Bahati ni kati ya maeneo yanayokumbwa na uhaba mkubwa wa maji katika kaunti ya Nakuru.