Mwanamume mwenye umri wa miaka 35 aliyejirusha baharini amedai ukosefu wa ajira ndio chanzo cha yeye kuchukua hatua hiyo.
Josephat Barongo, alijirusha baharini siku ya Alhamisi alipokuwa ameabiri ferry ya MV Kwale.
Baada ya kuhojiwa na maafisa wa usalama, Barongo alitaja ukosefu wa ajira na kutokuwa na familia ndio sababu za yeye kutaka kujitoa uhai.
“Sina kazi wala familia, heri nijirushe baharini niangamie kabisa,” alisema Barongo.
Akithibitisha tukio hilo, mkuu wa polisi eneo la Likoni Willy Simba alisema visa vya watu kujirusha baharini katika kivuko cha ferry cha Likoni vimeongezeka katika siku za hivi karibuni.
“Visa hivi vimezidi kushuhudiwa katika kivuko cha Likoni, itabidi hatua za haraka kuchukuliwa kudhibiti visa hivi,” alisema Simba.
Alisema kuwa mshukiwa huyo anatajiriwa kufikishwa mahakani na kufunguliwa shtaka la kutaka kujitoa uhai.