Viongozi wa kidini wamesema ya kwamba ukosefu wa haki, ukweli na amani ndicho chanzo kikuu cha migogoro.
Wakizungumza na waandishi habari mjini Nakuru jumanne wakati wa kongamano la mazungumzo ya kidini, katibu mkuu wa baraza la mkusanyiko wa dini (inter-religious council) kanda ya kati mwa bonde la ufa, Arch Deacon John Kimani wa dhehebu la kianglikana alisisitiza kuwa iwapo matatu hayo hayatazingatiwa kikamilifu, taifa hili litakosa maendeleo.
Kimani aliongeza kuwa ukosefu wa haki, ukweli na amani unasababishwa na tamaa ya baadhi ya viongozi, sawa na ukosefu wa maadili.
Ni matamshi yaliyoungwa mkono na naibu mwenyekiti wa baraza hilo Ali Hajji Abdi.
Kwa upande wake, Abdi aliwahimiza viongozi kuweka kando tofauti zao za kisiasa na badala yake wahakikishe wananchi wanahudumiwa kisheria.
Baadhi ya wale waliyoshiriki kongamano hilo la siku mbili, kutoka kwa dini mbalimbali waliunga kauli hiyo.
Hata hivyo viongozi hao sawa na waakilishi wa dini mbalimbali katika kongamano hilo kutoka kanda hii, wameapa kuhubiri amani katika maeneo yao.