Naibu gavana wa kaunti ya Nyamira Amos Nyaribo amesema kwamba changamoto za ukosefu wa fedha katika serikali za kaunti nchini huchangiwa sana na wizi wa mali ya umma na baadhi ya viongozi wakuu serikalini. 

Is there a story unfolding in your community? Let Hivisasa know

Akihutubu kwenye hafla ya kuadhimisha siku ya chakula duniani eneo la Rigoma kaunti ya Nyamira siku ya Ijumaa, Nyaribo alinukuliwa akisema kuwa serikali za kaunti hushindwa kulipa wafanyikazi wake kwa sababu ya wizi wa pesa na baadhi ya viongozi ambao huzificha kwenye akaunti za benki katika mataifa ya kigeni. 

"Serikali nyingi za kaunti hushindwa kuwalipa wafanyikazi wao kwa sababu baadhi ya viongozi nchini hujihusisha na wizi wa pesa za umma ambazo hufichwa kwenye akaunti za benki katika mataifa ya kigeni," alisema Nyaribo. 

Naibu huyo wa gavana aidha alisema kuwa yafaa serikali ya kitaifa kuweka maslahi ya wafanyikazi wa umma mbele badala ya kulipa madeni inayokopa kutoka mataifa ya kigeni ili kusaidia katika kuendeleza miradi mbalimbali nchini. 

"Yafaa serikali ya kitaifa iwape wafanyikazi wa umma kipau mbele kwa kuwalipa mishahara yao kwa wakati unaofaa badala ya kuweka mbele ulipaji wa madeni ya pesa za kigeni zinazokopwa ili kuendeleza miradi mbalimbali nchini," alihoji Nyaribo. 

Akizungumzia swala la kuwekwa mikakati ya kuhakikisha kuwa hali hiyo ya wizi wa pesa za umma inakabiliwa vikali, naibu huyo wa gavana alisema kuwa sharti washirikishi wa maendeleo washirikiane na serikali kuu ili kusaidia katika kutambua mianya ya wizi wa pesa za umma nchini.

"Ili changamoto za kuziba mianya ya pesa za umma nchini kutatuliwa, sharti washirikishi wa maendeleo washirikiane na taifa letu kuhakikisha kuwa hali hiyo ya uporaji wa mali ya umma inazuiwa," aliongeza Nyaribo. 

 Kwa muda sasa serikali nyingi za kaunti zimekuwa na changamoto za kulipa mishahara ya wafanyikazi wake kwa wakati unaofaa kutokana na serikali ya kitaifa kukosa kutuma pesa hizo kwa kaunti husika.