Ukosefu wa sheria mwafaka umeathiri kasi ya maeendeleo katika kaunti ya Nakuru, Seneta James Mungai amesema.
Kulingana na Mungai, wabunge wa kaunti hawajaweza kupitisha sheria ambazo zinaweza kuwavutia wawekezaji kuja katika kaunti ya Nakuru.
Akiongea Jumanne asubuhi katika afisi yake mjini Nakuru, Mungai alisema kuwa wabunge wa kaunti wamejihusisha sana na masilahi yao ya kibnafsi, na kusahau kuunda sheria za kuwezesha maandeleo katika kaunti hiyo.
“Kaunti yetu ina raslimali nyingi sana ambazo zikitumiwa vizuri zinaweza kutuletea utajiri mwingi, lakini watu tuliowachagua kuunda sheria za kaunti wamesahau kazi yao na hii imekwamisha maendeleo katika kaunti,” alisema Mungai.
Alisema kuwa hata kaunti ikiwa na raslimali na pesa za kutosha, haitaweza kuendelea iwapo hapatakuwa na sheria madhubuti za kuwezesha maendeleo.
“Kuleta maendeleo sio tu kuwafukuza wachuuzi kutoka mjini bali ni kuunda nafasi za kazi na kujenga viwanda ili kupunguza viwango vya umaskini na hilo litafanyika tu iwapo pataundwa sheria za kuwezehsa mambo hayo,” alisema Mungai.
Aliwashtumu wabunge wa bunge la kaunti kwa kuweka tumbo zao mbele, akisema kuwa wamekihusisha zaidi na kujitafutia utajiri na kusahau kuwahudumia raia waliowachagua.
“Wengi wa wabunge wa bunge la kaunti wamejiongezea utajiri mwingi tangu wachaguliwe na kazi yao imekuwa ni kutafuta mali ya kibnafsi kuliko kuwatafutia raia mali,” alisema Seneta huyo.