Do you have a lead on a newsworthy story? Share news tips with us here at Hivisasa!

Baraza la maimam na wahubiri katika kanda ya North-Rift limesema ukosefu wa uaminifu katika ndoa umechangia katika ongezeko la watoto ambao wanatelekezwa nchini.

Baraza hilo lilisema kuna haja ya wazazi kuhamasishwa kuhusu athari za kutelekeza watoto.

Mwenyekiti wa baraza hilo Sheikh Abubakar Bin alikosoa baadhi ya matangazo ya biashara kuhusu condom al maarufu 'weka condom mpangoni' ambayo anadai yanaonekana kuunga mkono ukosefu wa uaminifu katika ndoa.

Akizungumza mjini Eldoret siku ya Jumanne wakati wa warsha kuhusu dhuluma dhidi ya watoto, Bin alisema dini yake haiungi mkono matangazo kama hayo kwa msingi kuwa tabia hiyo haina maadili mema mbali na kukosea heshima taasisi ya ndoa.

“Dini yangu inaruhusu mwanamume kuoa wake zaidi ya mmoja iwapo haridhiki na mke badala ya kujihusisha na mpango wa kando,” alisema Bin.

Msimamo wa baraza hilo unawadia wakati ambapo idadi ya watoto ambao hutelekezwa mjini Edoret inazidi kuongezeka.

Afisa wa maswala ya watoto katika kaunti ya Uasin Gishu Bi Diana Komen alisema changamoto hiyo pia inachangiwa na ongezeko la mimba nje ya ndoa.

Bi Komen alisema wengi wa watoto hao huzaliwa na wasichana wadogo ambao hawako katika ndoa na huishia kutelekeza watoto hao wanaposhindwa kumudu matakwa yao.