Mwanamume aliyenaswa na maafisa wa polisi kutoka kituo cha feri kwa kosa la kujirusha baharini, amesema kuwa alikuwa mlevi wakati wa kutekeleza kitendo hicho.
Benson Mungai, alijitosa baharini siku ya Jumatatu alipokuwa ameabiri feri ya MV Nyayo.
Mungai alikubali shtaka hilo siku ya Jumanne mbele ya Hakimu Francis Kiambia na kusema kuwa ulevi ndio uliomsababisha kujirusha baharini.
“Nilikuwa mlevi siku hiyo wala sikufahama nafanya nini,” alisema Mungai.
Hata hivyo, akizungumza baada ya mwanamume huyo kukamatwa, Mkuu wa polisi eneo la Likoni Willy Simba alisema kuwa hiyo haikuwa mara ya kwanza kwa Mungai kujirusha baharini.
Kulingana na Bwana Simba, Mungai alijirusha baharini mwishoni mwa mwezi wa tano, na kufikishwa mahakamani alipoachiliwa kwa masharti.
Mahakama itatoa uamuzi wake tarehe Septemba 15, 2016.
Mungai aliokolewa na maafisa wa uogoleaji muda mfupi tu baada ya kujirusha majini.