Serikali imehimiza uma kutowatenga walemavu na kuwanyima uhuru wa kufurahia haki za kimsingi nchini, na badala yake kuwasaidia ili kupata huduma katika afisi mbali mbali za serikali kirahisi.
Wito huu ulitolewa na viongozi wakati wa kuadhimisha siku ya kimataifa ya walemavu.
Kamishna msaidizi wa jimbo, Anjella Wanyama, ambaye aliongoza sherehe za kuadhimisha siku wa walemavu wilayani Molo amesema serikali imekuwa mstari wa mbele kutambua na kusaidia wananchi wenye ulemavu ili kujimudu kimaisha.
Wanyama ambaye alitoa hotuba kwa niaba ya waziri wa leba na huduma za kijamii, Kazungu Kambi, alisema serikali inanuia kuwahusisha watu wote wenye upungufu wa kimaumbile katika nyanja zote za uongozi inapotimiza malengo ya Ruwaza 2030.
“Ni sharti walemavu wapewe nafasi ya kuhudumu katika afisi za umma na pia kupata haki za kimsingi badala ya kutengwa na kudhulumiwa,” Wanyama akasema.
Aliwapa changamoto wazazi wenye watoto walemavu kutambua vipawa walivyonavyo watoto hao na kuwapa nafasi ya kujimudu kimaisha bila kutatizwa.
Aidha mwenyekiti walemavu wilayani Molo, John Mugo, amesema inasikitisha kuona baadhi ya wazazi wanazidi kuwaficha na kuwatenga watoto walemavu huku wengine wakiteswa na kuishi maisha ya ukiwa.
Amesema watoto wote wanapaswa kupewa nafasi ya kufurahia haki za kimsingi na kutangamana na wanachi wote bila vikwazo kutoka kwa jamaa zao.
Mugo ameuliza serikali kuu na zile za kaunti kutekeleza mapendekezo ya kuyapa makundi ya vijana, kina mama na walemavu asilimia 30 ya zabuni akisema tenda hizo zimekuwa zikinufaisha wananchi wasiokuwa katika orodha ya wale wenye mahitaji mengi.