Umaskini unaosababishwa na ukosefu wa ajira umetajwa kama chanzo kikuu cha vijana wengi kujiunga na makundi yenye itikadi kali nchini, hasa katika eneo la Pwani.

Share news tips with us here at Hivisasa

Akizungumza siku ya Jumatano, katika eneo la Likoni kwenye kongamano la kuhamasisha vijana kuhusu athari za kujiunga na makundi ya kigaidi, mtaalamu wa maswala ya kijamii na mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Karatina, Dkt Peter Karari, alisema ni jukumu la serikali kutatua tatizo la umaskini na ukosefu wa ajira.

Alisema kuwa serikali inapaswa kuangazia suala hilo kwa haraka kwa kuwa changamoto hiyo ni sababu mojawapo ya makundi hayo kuchipuka.

Aidha, aliitaka serikali isuluhishe dhuluma zote za kihistoria kwa njia ya haki na usawa.

Vile vile, alitaja suala la uongozi duni, matumizi ya dawa za kulevya na matumizi mabaya ya mitandao ya kijamii kuwa sababu zinazochangia kuchipuka kwa makundi ya itikadi kali.

Kauli ya Karari inajiri baada ya kushuhudiwa kwa vijana wengi kujiunga kwenye makundi ya kigaidi pasi kujali athari zake.