Unyakuzi wa ardhi ya umma na mali ya serikali ya kaunti ya Kisumu, ni donda sugu huku uovu huo ukidaiwa kutekelezwa na watu mashuhuri katika kaunti hiyo.
Kulingana na meneja wa jiji la Kisumu Doris Ombara, unyakuzi wa ardhi na mali ya serikali ya kaunti ya Kisumu unawahusisha baadhi ya wanasiasa, na hata baadhi ya viongozi wa kidini, kwenye kaunti hiyo.
Ombara alisema idadi kubwa ya ardhi zilizotengewa maendeleo ya jiji la Kisumu tayari zimenyakuliwa, na hivi karibuni serikali ya kaunti ya Kisumu itakosa sehemu ya kuwauzia waekezaji ili kufanikisha miradi ya maendeleo.
“Tangu nije jijini Kisumu miezi sita iliyopita, nimejaribu kujiepusha kabisa na suala la ardhi inayomilikiwa na serikali ya kaunti.
Unyakuzi wa ardhi ni suala nyeti sana kwa sababu linahusisha viongozi wa kisiasa, kidini na wataalamu mbali mbali, ambao hawafai kuguswa na yeyote,” akasema Ombara.
Kwenye kikao na wanahabari jijini Kisumu mapema Jumatatu, Ombara alisema kuwa aliamua kujitenga na suala la ardhi, kwa sababau ‘hangeenda popote’ iwapo angejaribu kuangazia suala hilo.
Meneja huyo alifichua kuwa hakuna ushuru unaokusanywa kutoka kwa mali ya serikali ya kaunti ya Kisumu ambayo imenyakuliwa, ilihali serikali hiyo inashtumiwa kwa ukusanyaji wa kiwango cha chini cha ushuru.
Alitoa wito kwa wenyeji wa jimbo la Kisumu, kushirikiana na wadau wengine katika kukomesha unyakuzi wa ardhi ya umma.