Seneti ya Chuo Kikuu cha Nairobi imeamua kuratibisha muda wa kuhudumu kwa viongozi wa muungano wa wanafunzi wa Sonu ili kuwapa wanafunzi wengi nafasi ya kuongoza.
Akizungumza siku ya Jumanne, Naibu wa Chansela Prof Peter Mbithi alisema kwamba wataunda kamati itakayoratibu katiba ya Sonu.
Bwana Mbithi alisema kuwa lengo la kufanyia katiba hiyo mabadiliko ni kuhakikisha kuwa muungano huo wa wanafunzi unawajibika zaidi kwa kuangazia mahitaji ya wanafunzi.
"Tulifanya mkutano mnamo Aprili 27, 2016, na Seneti ikapendekeza uteuzi wa kamati itakayoratibu katiba ya Sonu," alisema Mbithi.
Aliongeza: "Mabadiliko yaliyopendekezwa ni pamoja na yafuatayo miongoni mwa mengine: Kuweka makataa kwa muda wa kuhudumu kwa viongozi wa Sonu ili wanafunzi wengi kupata nafasi ya kuongoza; Kupunguza faida na mafao kwa viongozi ili kupunguza mvutano kati ya washindi na washindwa."
Kamati hiyo pia itafanyia mabadiliko kiwango cha gharama za kampeni za nafasi mbalimbali katika muungano huo wa wanafunzi.
Mkutano huo pia ulipendekeza kupunguzwa kwa jukumu la viongozi walio madarakani katika usimamizi wa uchaguzi.
Kubuniwa kwa vigezo vya uteuzi kwa wagombeaji pia kulipendekezwa ili kukuza uongozi wenye maadili na utaalamu.
Mapendekezo haya yanajiri baada ya kushuhudiwa ghasia katika chuo hicho kikuu baada ya madai ya wizi wa kura kuibuka.
Mike Jacobs, ambaye alidai kuwa aliibiwa kura wakati wa uchaguzi wa Sonu kwa manufaa ya Paul Ongili, al maarufu Babu Owino, alikuwa miongoni mwa wanafunzi 33 ambao walifurushwa kutoka chuoni humo baada ya ghasia hizo zilizosababisha afisi za Sonu kuteketezwa.
Wanafunzi 201 walisimamishwa kwa muda kuendelea na masomo kufuatia machafuko hayo.