Upepo mkubwa uling’oa paa la kanisa moja pamoja na boma la mkaazi katika eneo la Free Area viungani mwa mji wa Nakuru mnamo Jumatatu.

Share news tips with us here at Hivisasa

Paa la kanisa hilo la Revival City Church liling’olewa mwendo wa saa nane adhuhuri wakati upepo mkali ulipovuma.

Wakaazi walielezea kuskia sauti kubwa kabla ya kushuhudia mabati ya majengo hayo mawili yakipeperushwa hewani huku mengine yakikwama katika nyaya ya stima na kusababisha hiltilafu za umeme.

“Upepo ulivuma mara moja tu. Tukaanza kushindwa tena ni nini hicho kinatoa masauti ya kutisha kama kitu kinabomolewa. Ghafla tukaona mabati yakipeperuka juu hewani watu wakaaza kukimbia kwa sababu mengine yalikwama kwenye stima,” Godfrey Maina alisema.

Walisema kuwa japo hamna aliyejeruhiwa kwenye mkasa huo, hofu yao ni kuwa iwapo hatua ya dharura haitachukuliwa huenda kukwama kwa mabati hayo kwenye nyaya za umeme kukasababisha moto.

Hata hivyo hadi wakati wa kuandika taarifa hii mwendo wa saa kumi na moja, maafisa kutoka kampuni ya umeme nchini KP tawi la Nakuru hawakuwa wametoa mabati hayo.