Rais Uhuru Kenyatta ameusuta mrengo wa upinzani nchini kwa kuwaingiza wakenya katika siasa potovu. 

Is there a story unfolding in your community? Let Hivisasa know

Akiongea huko Njoro, kaunti ya Nakuru katika hafla ya kuchangisha pesa shuleni humo siku ya Jumapili, Rais alisema upinzani si uadui wala kutusi wenzako kila wakati. 

"Mimi nawaambia wale ndugu zangu kuwa upinzani ni mzuri, lakini tupingane katika sera, maendeleo na mambo mengine ya manufaa kwa wakenya lakini si kutugawanyisha kisiasa, kikabira au kutokana na dini," alisema Rais. 

Haya yanajiri siku mbili tu baada ya wabunge wanane wa ODM chini ya muungano wa CORD kuzua vurumai bungeni wakati Rais alikuwa anahutubia kikao maalum cha bunge la seneti na la kitaifa. 

Gavana wa Nakuru, Bw. Kinuthia Mbugua alisema huko ni kumkosea Rais heshima kama kiongozi aliyechaguliwa kihalali chini ya katiba.

"Ni jambo la kusikitisha kuona watu wakimpigia Rais kelele na firimbi bungeni. Lakini tulifurahi kuona Rais hukukasirika, bali ukiwacheka na kusema ni sarakasi," alisema Gavana Mbugua. 

Hii ni mara ya pili kwa Rais kuzuru Nakuru baada yake na naibu wake, William Ruto kuzuru kaunti hii kwa ziara ya siku mbili ambapo walizindua miradi kadhaa ya maendeleo. 

Mbunge wa Nakuru Town mashariki David Gikaria pia aliwasuta wanasiasa wa mrengo wa upinzani kwa shairi lake 'Unnecessary Whistlebrowing'.