Chama cha kisiasa cha URP kinatathmini pendekezo la kujiunga na chama cha Jubilee Alliance kabla ya kutoa uamuzi wa mwisho.
Akizungumza mjini Nakuru, mbunge wa Kuresoi Moses Chaboi alisema URP kinatathmini iwapo kitavunjwa na kuungana na JAP, au kisalie kama chama cha kujitegemea.
Cheboi alisema wanachama wa URP wana wasiwasi kuwa huenda wakatengwa iwapo kitavunjiliwa mbali.
Mbunge huyo alisema kuwa wanafuatilia kwa makini uchunguzi wa maafisa wa serikali wanaohusishwa na ufisadi, akiongeza kwamba serikali ina njama ya kuwataja wanachama wake kama wafisadi.
Chama cha URP, chenye kauli mbiu 'Kusema na Kutenda' kinaongozwa na naibu wa raisi William Ruto.
Chama cha Jubilee Alliance kiliundwa baada ya kuvunjiliwa mbali muungano wa Jubilee, huku URP na TNA vikiwa mojawapo ya vyama tanzu na vikuu vya muungano huo.
JAP ilianza maisha vibaya, baada ya kupoteza katika uchaguzi mdogo wa Kajiado ya Kati, ambapo kilipata ushindani mkali kutoka kwa chama cha ODM.
Raisi Uhuru Kenyatta anatarajia kutumia tiketi ya JAP kuwinda uungozi wa nchi kwa kipindi cha pili katika uchaguzi mkuu ujao wa mwaka wa 2017.