Kufungwa kwa afisi za ardhi katika kaunti ya Kisii kumepeana nafasi kwa kuwekwa kwa mpangilio mzuri na ulainishaji wa stakabadhi muhimu kulingana na waziri wa ardhi na miundomsingi ya kaunti Moses Onderi.

Share news tips with us here at Hivisasa

Alikuwa akiyasema haya katika afisi zake siku ya Ijumaa wakati akitoa ripoti kuhusu yale ambayo yameafikiwa kutokana na amri iliyotolewa na waziri wa ardhi Fred Matiangi alipomtembelea gavana James Ongwae juma moja lililopita.

Onderi alisema kuwa changamoto ambayo wamekumbana nayo ni mpangilio mbaya wa stakabhadhi mhimu za mashamba, jambo ambalo kulingana naye lilikuwa likifanywa maksudi ili mwanya wa rushwa kuwepo katika utafutaji wa baadhi ya faili muhimu.

“Kwa utoaji wa huduma bora kwa wananchi sharti mipangilio mwafaka ifanywe kuzuia urundikaji wa stakabadhi muhimu kwa njia isiofaa,” alisema Onderi akiwatembeza waandishi wa habari katika afisi hizo ambapo wahudumu wanaendelea kufanya faili.

Kulingana naye, hii awamu ya kwanza ya majuma mawili ni kupanga faili hizo kwa njia inayofaa na katika viekezi vipya, huku awamu ya pili ikiwa ya kuweka stakabadhi hizi kwa mfumo wa kidijitali kuepusha misukosuko ya hapa na pale kuhusu mashamba.

Afisa wa wizara ya ardhi David William alisema kuwa wizara inafuatilia kwa makini jinsi shughuli za mashamba zinavyotatuliwa kaunti ya Kisii, kabla ya kwenda katika kaunti zingine mkoani nyanza kuepusha mkinzano ambao umekuwa ukishuhudiwa hapo awali.