USAID ikishirikiana na mashirika mengine nchini imeandaa warsha itakayowakutanisha pamoja walimu na wanafunzi kutoka shule mbalimbali Mombasa, kujadili maswala ya elimu na uongozi.

Is there a story unfolding in your community? Let Hivisasa know

Warsha hiyo chini ya mradi unaofahamika kama SHIRIKI inalenga kutoa mafunzo kwa wanafunzi kuhusu maswala ya ugatuzi na pia kuwatayarisha katika maisha ya usoni baada ya shule.

Mshirikishi mkuu wa mradi huo Salvanos Awuori, amesema lengo kuu ni kuhakikisha wanafunzi wanafahamu mambo ya ugatuzi wakiwa bado shuleni, ili kuwasaidia kutatua matatizo ya uongozi yanayoshuhudiwa nchini.

“Tunajaribu kuona kwamba wao pia wanaelewa ugatuzi ni nini, kwa sababu tunajua kwamba uongozi umegatuliwa hata kule shuleni, ambapo wanafunzi wanapewa fursa ya kujiongoza wenyewe,” alisema Awuori.

Mradi wa SHIRIKI unalenga Kaunti nne za ukanda wa Pwani ikiwa ni pamoja na Mombasa, Kwale, Tana River River na Kilifi.

Katika kila warsha inayoandaliwa wakati wa likizo, wanafunzi watano na mwalimu mmoja huchaguliwa kutoka shule mbalimbali na kisha kukutanishwa pamoja kwa siku tatu na kupewa mafunzo hayo.

Warsha ya Mombasa iliyoanza Jumapili na inayotarajiwa kukamilika siku ya Jumanne inafanyika katika Shule ya upili ya Shimo la Tewa.

Warsha hiyo imeshirikisha wanafunzi 50 na walimu 10 kutoka shule tofauti.

Wanafunzi waliozungumza na mwandishi huyu wametaja utumizi wa mihadarati kama kikwazo kikubwa kwa vijana, jambo wanalosema linazima ndoto ya vijana wengi kuwa viongozi siku za usoni.

“Tunaishi na wahalifu lakini hatutaki kusema, na hiyo ndio sababu mihadarati inazidi kuenea. Nawashauri wanafunzi wenzangu kuwataja wale wanaohusika bila kuogopa,” alisema Ruth Mwihaki, mwanafuzi wa kidato cha pili katika Shule ya upili ya Star of the Sea.

Mshirikishi wa mradi huo Salvanos Awuori alisema wanalenga kuwafikia wanafunzi 5,000 kabla ya mwaka ujao wa 2017.