Idara ya Usalama katika Kaunti ya Mombasa imesema kuwa imeongeza idadi ya maafisa wa usalama wanaoshika doria katika taasisi zote za elimu katika kaunti hiyo, kutokana na ripoti za tishio la ugaidi, walizopokea kutoka kwa idara ya ujasusi.
Akiwahutubia waandishi wa habari afisini mwake siku ya Alhamisi, Mkuu wa polisi katika kanda ya Pwani Francis Wanjohi, alisema kuwa tishio hizo zilikuwa zimetolewa dhidi ya taasisi za elimu.
Alisema kuwa haijulikani ni wapi haswa panalengwa na imebidi taasisi zote kupewa maafisa wa polisi.
“Imebidi tuweke maafisa wa polisi kwenye taasisi hizo. Kwa mfano, maafisa wa usalama katika Chuo cha Ufundi cha Mombasa wamezidishwa kutoka watano hadi 15,” alisema Wanjohi.
Taasisi zingine zilizo ongezewa maafisa wa usalama ni pamoja na Chuo cha KMTC na Chuo cha Ufundi cha MTTI.