Kamati ya usalama katika Kaunti ya Mombasa imeweka mikakati ya kuzuia kuzuka kwa visa vya uchomaji wa shule vinavyoendelea kushuhudiwa kote nchini.

Is there a story unfolding in your community? Let Hivisasa know

Kamishna wa Kaunti ya Mombasa Maalim Mohamed ameagiza kamati za usalama pamoja na wadau katika sekta ya elimu kuandaa vikao kutafuta mbinu za kuzuia visa hivyo kushuhudiwa Mombasa.

Akizungumza na wanahabari ofisini mwake, Maalim alisema kuwa usalama utaimarisha katika shule za mabweni na taasisi nyengine za elimu.

“Nimeagiza manaibu kamishna wote kufanya mkutano na wakuu wa shule zote za upili katika kaunti hii pamoja na wakurugenzi wa elimu ili kutafuta suluhu ya kuzuia visa kama hivi kutokea katika kaunti yetu,” alisema Maalim.

Aidha, kamishna huyo amesisitiza kuwa kanuni zote za hivi karibuni zilizobuniwa na Waziri wa elimu nchini Fred Matiang'i lazima zitekelezwe ipasavyo.

Haya yanajiri baada ya kuendelea kushuhudiwa uchomaji wa shule katika maeneo mbali mbali ya taifa huku katibu mkuu wa muungano wa walimu Knut Wilson Sossion akiitaka wizara ya elimu kufunga shule zote mapema ili kuzuia shule zaidi kuathirika.