Naibu OCPD wa Kisauni Walter Abondo amesema eneo hilo lililogonga vichwa vya habari kwa utepetevu wa usalama unaotekelezwa na makundi ya Wakali Kwanza na Wakali Wao sasa ni salama kwa wenyeji na wafanyabiashara.
Akizungumza kwenye mahojiano ya moja na moja, Abondo alisema kwamba tangu visa vya utovu wa usalama kuanza kuibuka eneo hilo, kumekuwa na mikakati dhabiti ya kuhakikisha kuwa magenge yote yanayowapora na kuwaua wananchi yanakabiliwa vilivyo.
Abondo alisema maafisa wanaoshika doria kila wakati eneo hilo wamesaidia pakubwa kuimarisha usalama, kwa kuwa kwa wakati huu wenyeji wanaweza kutembea nyakati za usiku bila ya kuvamiwa wala kuporwa.
“Kamati iliyoundwa na Kamishna wa Mombasa Maalim Mohamed inayojumuisha OCPD wote na wazee wa mitaa imekuwa ikifuatilia kwa karibu mienendo ya magenge hayo. Kwa sasa tumewakabili baadhi ya wahalifu na hata kuwatia mbaroni,” alisema Abondo.
Abondo pia alisema kuwa wanashirikiana na wananchi ambao hutoa taarifa moja kwa moja katika vituo vya polisi wakati wanaposhuhudia kisa chochote kinachohusiana na maswala ya usalama.
Hata hivyo, amewaomba wazazi kushirikiana na idara ya usalama kuhakikisha wanao waliojiunga na makundi hayo wanarudi katika jamii na kuanza kushiriki miradi ya maendeleo kwa manufaa yao wenyewe.