Naibu kamishena wa kaunti ya Kisii Phillip Soi amesema maafisa wa polisi katika kaunti hiyo wamejitayarisha vilivyo kwa usalama hasa wakati wa maonyesho ya kilimo ambayo yatafanyika katika uwanja wa Gusii stadium wiki ya pili mwezi wa saba mwaka huu.
Akiongea leo katika mji wa Kisii kamishena huyo alisema lazima wakaazi wa kaunti ya Kisii wahakikishiwe usalama wa kutosha ili vurugu yoyote isifanyike kwa wakaazi hao.
“Sisi kama wanakamati wa masuala ya usalama katika kaunti ya Kisii lazima tujitayarishe kuweka usalama wa kutosha kwa wakaazi wa eneo hili. Lazima tuajibike kwa usalama kila wakati,” alisema Soi.
Aliongezea: “Mikakati hiyo ya kuweka usalama wakati wa maonyesho ya kilimo na baada ya maonyesho hayo tayari imekamilika na tunawahakikishia wale watakuja kwa maonyesho hayo usalama uko ngangari. Visa vya uhalifu havitashuhudiwa katika eneo hili.”
Wakati huo huo, mwenyekiti wa maonyesho hayo kaunti ya Kisii Julius Bosire amewaomba watu wa kuonyesha maonyesho hayo kuja kwa wingi huku akisema ana imani kuwa watu watakuja wengi kushinda mwaka jana.
“Noamba mwaka huu watu wa kuonyesha maonyesho hayo watakuja kwa wingi kuliko wale waliokuja mwaka jana. Wakaazi wote mumekaribishwa kuja kwa maonyesho maana tayari kila kitu kimewekwa tayari,”alisema Bosire.