Maafisa wa polisi mjini Mombasa wamewahakikishia wakazi wa eneo hilo kuwepo kwa usalama dhabiti licha ya kuwa na hofu huenda eneo hilo likavamiwa na magaidi.
Afisa mkuu wa Polisi Kisiwani Mombasa Martin Asin amesema kuwa maafisa wa polisi wametumwa kushika doria kikamilifu ili kuzuia kushuhudiwa kwa visa vya kihalifu huku akiwataka wakazi kutokuwa na hofu ya kiusalama.
Akiongea na wanahabari afisini mwake siku ya Jumatatu, Asin amesema kuwa maafisa wa polisi wako macho kuhakikisha kuwa hakuna mtu yeyote anavuruga usalama wa eneo la Mombasa na akaonya kuwa atakayepatikana akijaribu kuzua hofu atakabiliwa.
"Kama idara tumetuma maafisa wetu wa polisi mashinani kuimarisha usalama na kuzuia hofu iliyoko kwa sasa kuwa Mombasa itavamiwa, hilo tunasema ni uvumumi tu, usalama uko sawa na wale watakaopatikana wakitoa hofu kwa wakaazi wataadhibiwa," alieleza Asin.
Asin amewataka wakazi kushirikiana na maafisa wa polisi katika kutoa habari muhimu kuhusu washukiwa wa uhalifu ili hatua za kisheria kuchukuliwa dhidi yao.
Kauli ya Asin imejiri siku mbili tu baada ya Waziri wa usalama wa ndani Joseph Nkaissery kuwaonya viongozi wa kisiasa dhidi ya kuwachochea vijana na kuzua vurugu.