Idara ya usalama imesema kuwa imeweka mikakati mwafaka ya kukabiliana na wahalifu wanaolenga kuzua vurugu, wakati wa maonyesho ya kilimo Kaunti ya Mombasa.

Share news tips with us here at Hivisasa

Naibu Kamishna wa kaunti ndogo ya Changamwe Benjamin Njoroge, amewataka wageni wanaolenga kuhudhuria maonyesha hayo kuondoa hofu, huku akiongeza kuwa polisi watakuwa macho kuhakikisha hakuna visa vya utovu wa usalama vitakavyo shuhudiwa.

Akizungumza na wanahabari siku ya Alhamisi, Njoroge alisema kuwa maafisa wa polisi wanashika doria saa 24 katika eneo la Changamwe.

Aidha, aliwataka wafanyabiashara pia kuondoa hofu, kwa kuwahakikishia kuwa usalama wao umezingatiwa.

Wakati huo huo, amewataka wakaazi, mabalozi wa Nyumba Kumi pamoja na wahudumu wa bodaboda kushirikiana na maafisa wa polisi katika kutoa habari kuhusu washukiwa wa uhalifu ili watiwe mbaroni.

"Tunawaomba wakaazi kushirikiana na maafisa wa polisi kuhakikisha kuwa usalama wa wananchi unaangaziwa vyema,” alisema Njoroge.